MKURUGENZI MKUU TAFORI DKT. REVOCATUS MUSHUMBUSI AZINDUA KAMATI YA MAADILI YA UTAFITI – TAFORI REC

Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania TAFORI Dkt. Revocatus Mushumbusi amezindua rasmi Kamati ya Maadili ya Utafiti ya TAFORI yaani TAFORI Research Ethical Committee itakayo pitia na kutathmini tafiti za misitu na nyuki zinazofanywa hapa nchini ili kusaidia kuwa na manufaa ya kisayansi, uhifadhi na Maadili.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Murira TAFORI Morogoro Julai 13, 2023, Dkt Mushumbusi alisema, kamati hii itasaidia katika kusimamia na kuhakikisha maadili ya utafiti yanafuatwa lakini pia kujua idadi ya tafiti zinazofanywa na zinafanyika wapi ndani ya nchi.

“Kabla ya kufanya tafiti, kamati lazima ijiridhishe kama tafiti hizo zinamaadili na machango wowote kwa nchi ili kuweza kupata takwimu za uhakika na zinafanyika wapi,” alisema Dkt. Mushumbusi.

Akiwa katika uzinduzi wa kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu TAFORI alisema, Kamati hii ni itasaidia kujua kama tafiti zimezingatia maadili ya Kitanzania, kama tafiti zinajibu vipaumbele vya nchi na dira ya maendeleo ya mwaka 2025, Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano na Mkakati wa Kukuza Uchumi na kupunguza umaskini.

Aliongeza kuwa kamati hii itasaidia kuibua mahitaji ya kitafiti na kuyafanyia kazi ili kujibu mahitaji ya wananchi, na Kuleta mchango mkubwa katika sekta ya misitu na nyuki lakini pia kuwa na msemaji mmoja kwenye mambo ya kitaalamu yahusuyo matumizi ya teknolojia bora ya uendelezaji misitu.

Kamati hii itakua na Jukumu la kusaidi kutoa taarifa za Kimaadili kwa mujibu wa kanuni za utafiti wa misitu za mwaka 2020, ikiwa na dhumuni la kulinda utu, haki, usalama na ustawi wa washiriki wa utafiti, kuhakikisha utafiti na matokeo ya utafiti yanakidhi matakwa na maadili ya kisayansi na sifa za uhifadhi.

Wajumbe walioteuliwa kwenye kamati hio ni pamoja na Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu Sokoine Dkt. Ezekiel Edward Mwakalukwa, Mtafiti Mkuu TAWIRI Dkt. Angela Mwakatobe, Afisa Uratibu Tafiti Mkuu COSTECH Dkt. Joseph William Maziku, Mkurugenzi wa Matumizi ya Misitu TAFORI Dkt. Chelestino Balama, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Climate Action Network Tanzania Dkt. Sixbert Mwanga, Afisa Misitu Mkuu TFS John Rutagwaba na Afisa Ufugaji Nyuki Mwandamizi Chuo cha Tabora Issa Mpinga.

Kamati hii iliteuliwa na Bodi ya Wakurugenzi wa TAFORI katika Kikao cha 32 kilichofanyika April 4, 2023 TAFORI Makao Makuu, Morogoro.