NASSARI AIOMBA TAFORI KUANDAA KONGAMANO LA KITAIFA KUDHIBITI MIMEA VAMIZI.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe. Joshua Nassari ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) pamoja na wadau wote wa sekta ya misitu kwa kupambana na mimea vamizi lakini pia kwakuwa na usimamizi mzuri katika kutoa mafunzo ya kupambana dhidi ya mmea vamizi aina ya Mrashia.

Mhe. Nassari ametoa pongezi hizo Mei 25, 2023 katika eneo la Mto wa Mbu Wilayani Monduli Arusha, wakati anahitimisha warsha ya muendelezo wa kusaidia utekelezaji wa Mkakati na Mpango kazi wa kupambana na kudhibiti mmea aina ya Mrashia katika maeneo ya Bonde la Ziwa Natron, kutokana na eneo hilo kuathirika sana na mmea huo ambao ni hatari kwa maeneo ya malisho, kilimo na kuathiri mfumo wa ikolojia ya maeneo hayo.

Kadhalika katika kikao hicho, kilichohudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Dr. Revocatus Mushumbusi, Mh. Nasari ameomba kuwepo kwa juhudi za kitaifa kwa wadau ili kuona namna ya kuandaa kongamano la kitaifa kama sehemu ya juhudi za pamoja za kudhibiti na kutokomeza mimea vamizi hasa Mrashia na si kwa Wilaya tatu tu bali nchi nzima.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli pia amesisitiza jamii kuendelea kushirikishwa katika kudhibiti na kuondokana na Mrashia ili kulinda vyanzo vya maji na mapori yanayotumiwa na wanyama pori.

Aidha Mkurugenzi Mkuu Dr. Revocatus Mushumbusi amewataka washiriki wa warsha hiyo kutumia elimu waliyoipata kutoka kwa watafiti wa TAFORI na wadau wengine kupambana dhidi ya mmea vamizi aina ya Mrashia usiendelee kuenea kwenye maeneo mengine.

Dr. Mushumbusi ametoa rai pia kwa wananchi kuwa makini na usafirishaji wa mimea vamizi kutoka eneo moja kwenda jingine ili kudhibiti usambaaji wake.

Wadau mbalimbali akiwemo mwanasayansi Mkuu kutoka CABI nchini Uswisi Dr. René Eschen ameomba kuwepo kwa Mfuko wa uwezeshwaji ili kupambana dhidi ya Mrashia.

Pamoja na hayo Mradi huu wa kupambana na mimea vamizi uliandaliwa na TAFORI kwa kushirikiana na Shirika la Sayansi na Utafiti wa Kilimo la Uswizi (CABI SWISS), Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA), Jukwaa la Maliasili Tanzania (TNRF), Huduma za Utafiti na Maendeleo kwa Jamii (CORDS) na wadau mbalimbali wanaozunguka bonde la ziwa Natron kwa lengo la kulinda baioanuai na rasilimali ambata hasa katika maeneo ya malisho dhidi ya mmea vamizi ikiwemo Mrashia.