TAFORI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA GATSBY AFRIKA KUENDELEZA SEKTA YA MISITU NCHINI

Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) imekubaliana kuendelea kushirikiana na GATSBY AFRICA katika kuendeleza sekta ya misitu kutokana na shughuli zilizokuwa zikifanywa na shirika la Forest Development Trust (FDT) kuhamishiwa GATSBY AFRICA ambalo ndio shirika lililoanzisha FDT.
Makubaliano hayo yalifanyika katika kikao cha pamoja Juni 18, 2023 katika ukumbi wa TAFORI Makao Makuu ikiwa ni muendelezo wa vikao vilivyofanyika baina ya TAFORI na GATSBY AFRICA.
Aidha, katika kikao hicho ilielezwa kuwa GATSBY AFRICA kupitia FDT iliweza kuanzisha majaribio 76, ambapo 71 ni ya miti aina ya Mikaratusi (Eucalyptus) na Matano ni miti aina ya Misindano (Pine). Baadhi ya majaribio hayo yamefanyiwa tathmini ya ukuaji pamoja na ubora wa mbao. Hata hivyo, GATSBY AFRICA imeridhia kufadhili tathmini ya majaribio yaliyosalia.
Pamoja na hayo GATSBY AFRICA kupitia FDT kwa kushirikiana na Taasisi za Misitu zilizoko ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo TAFORI , zilitengeneza mfumo wa kubaini spishi mbalimbali za miti na mahali zinapostahili kupandwa (Site Species Matching Tool).
Ili kuongeza kasi ya matumizi ya mfumo huu GATSBY AFRICA iliridhia kutoa mafunzo kwa Watumishi na Watafiti wa TAFORI mwishoni mwa mwezi Julai ili kuwajengea uwezo zaidi.