TAFORI, KEFRI ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA UTAFITI KUENDELEZA TEKNOLOJIA ZA *KILIMO MISITU KATIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Morogoro, Julai 28, 2026. Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na Taasisi ya Utafiti wa Misitu ya Kenya KEFRI katika sekta ya utafiti kwa lengo la kuboresha uzalishaji endelevu wa miti ya mikorosho, ili kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo ya ukame.

Akifungua kikao hicho kilichofanyika Julai 28, 2026 Makao Makuu ya TAFORI, Morogoro, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, alieleza kuwa ushirikiano wa taasisi za utafiti ni muhimu katika kuzalisha maarifa, teknolojia na ubunifu unaoweza kutoa suluhisho kwa changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo na misitu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika kikao hicho, Meneja wa Utafiti wa Uzalishaji Misitu TAFORI, Dkt. Numan Amanzi, alifanya mawasilisho ya shughuli mbalimbali za utafiti zinazotekelezwa na TAFORI ili kuangalia maeneo yenye fursa za kuendeleza ushirikiano kati ya taasisi hizo.

Aidha, aliwasilisha maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Maendeleo ya Mifumo Endelevu ya Uzalishaji wa Miti ya Mikorosho kwa Ajili ya Kuboresha Maisha na Kuimarisha Ustahimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi katika Maeneo Kame ya Kenya na Tanzania. Aidha, kupitia teknolojia za kilimo misitu, miti ya mikorosho ina fursa katika biashara ya kaboni, hivyo kuongeza mazao ya mti huu, mbali na korosho.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Dkt. Amanzi alisema kuwa mradi huo unalenga kukabiliana na kushuka kwa uzalishaji wa zao la korosho kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mradi huu utaenda kuhamasisha uzalishaji endelevu na unaozingatia mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda kati ya Tanzania na Kenya.

Dkt. Amanzi, alisema mradi huu unatekelezwa katika Wilaya za Tandahimba na Manyoni, Tanzania, huku nchini Kenya, ukitekelezwa katika Kaunti za Kwale na Kilifi. Ambapo utafiti wa awali umehusisha kaya 180 za wakulima waliosajiliwa kama wanufaika wa mradi kwa lengo la kuweka taarifa za msingi zitakazotumika katika ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mradi

Akihitimisha kikao hicho, Dkt. Mushumbusi aliwashukuru washirika kutoka Kenya hususan KEFRI, kwa kutembelea TAFORI na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano huo katika kubadilishana uzoefu, maarifa na teknolojia, hususan katika tafiti na matumizi ya teknolojia za kukabiliana na moto wa misitu ili kuimarisha usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za misitu katika nchi zote mbili.

Mradi huu unasimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Kenya (KEFRI), kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) pamoja na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Dedan Kimathi (DeKUT).