Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imepokea na kujadili taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu utendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI).
Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Timotheo Mnzava, imepokea taarifa hiyo leo Agosti 18, 2026, Bungeni Jijini Dodoma, ambapo imeishauri Wizara kupitia TAFORI kuendelea kuimarisha utafiti unaolenga kuongeza thamani ya mazao ya misitu na kuwezesha uzalishaji wa bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa.
Vilevile, Kamati imeishauri Wizara kupitia TAFORI kuja na mpango utakaowezesha kuanzishwa kwa viwanda vitakavyokuwa vya mfano katika uzalishaji wa mazao ya miti ili waweze kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya soko kitaifa na kimataifa na kuhakikisha bidhaa hizo zinapatikana na kutangazwa.
Kamati hiyo imesema inatambua na kuthamini mchango wa utafiti unaofanywa na TAFORI katika sekta ya misitu, hususani katika kuzalisha maarifa yanayoweza kutumika katika kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali za misitu.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge kuwa Wizara itaendelea kuziwezesha taasisi zake ili ziendelee kufanya kazi zake kwa ufanisi na kufikia malengo yanayotarajiwa.
Kadhalika, ameiambia kamati hiyo kuwa Wizara na wataalamu wake wapo kazini kila wakati kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuifanya Sekta ya Maliasili na Utalii kundelea kuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa wananchi na taifa kwa ujumla.