NAIBU WAZIRI MHE. CHANDE AZINDUA BODI YA WAKURUGENZI YA TAFORI

Aagiza TAFORI kudhibiti Mioto misituni kupitia tafiti.

Agiza TAFORI kusimamia tafiti zenye kutoa majibu ya usimamizi bila kuleta kero kwa Watalii

Morogoro. Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) imeelekezwa kuzipa kipaumbele tafiti za kubaini viashiria vya moto wa misitu mapema na kuboresha usimamizi wa moto katika maeneo ya hifadhi, ili kulinda misitu, bioanuai na shughuli za utalii.

Maagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Chande (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) hii leo Septemba 21, 2026 TAFORI Makao Makuu, Morogoro wakati akizindua rasmi Bodi ya 13 ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) ambapo amesema tafiti zinapaswa kutoa majibu ya kisayansi kuhusu moto unaotumika kama sehemu ya usimamizi wa maeneo ya hifadhi, pamoja na njia za kuzuia moto usio wa lazima na kutoa tahadhari mapema.

“Mtaungana nami kuwa wadau wa misitu na ufugaji nyuki wanakabiliwa na changamoto ambazo zinahitaji majawabu. Mfano moto wa msituni unaojitokeza na kuathiri ukuaji wa miti, lakini pia upo moto unaoanzishwa katika maeneo ya hifadhi umeleta kero kwa watalii,” amesisitiza Mhe. Chande.

Aidha, Naibu Waziri Chande ameielekeza TAFORI kuongeza uwezo wa maabara za ndani kupima usalama na ubora wa asali, akisema Tanzania inalenga kutumia fursa ya masoko ya nje, ikiwamo Ulaya, bila kulazimika kupeleka sampuli nje ya nchi. Amesema uwezo huo utapunguza gharama za vipimo na kuongeza ushindani wa asali ya Tanzania.

“Niwaombe Bodi inisaidie kuhakikishakuwa sampuli za utafiti zinapimwa katika maabara za hapa nchini ili kupunguza gharama na kuongeza nguvu ya ushindani katika soko,” amesema Mhe. Chande

Naibu Waziri Chande ameitaka Bodi hiyo kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taasisi wa Miaka Mitano (2026/27 – 2030/31) ili kuhakikisha unazingatia utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, kusimamia uwajibijikaji na nidhamu kwa watumishi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, amesema Taasisi itatekeleza maelekezo ya Wizara na kuendelea kuimarisha tafiti zenye tija kwa uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na nyuki.

Amesema TAFORI pia itaendelea kujenga uwezo wa watafiti kupitia mafunzo ya elimu ya juu na uzoefu wa ndani na nje ya nchi, huku ikiimarisha ushirikiano na taasisi za kitaifa na kimataifa katika tafiti za misitu na ufugaji nyuki.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi walioteuliwa, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Verdiana Grace Masanja, ni pamoja na Dkt. Revocatus Petro Mushumbusi, ambaye ni Katibu wa Bodi; Bw. Daniel Charles Pancras; Prof. Dos Santos Aristariki Silayo; Dkt. Amos Mahunda Nungu; Bi. Felister Steven Lelo; Prof. Donatha Damian Tibuhwa; Bw. Jasper Lazaro Makala; pamoja na CPA. Beatrice Musa Lupi