TAFORI YATOA MAFUNZO YA KUREJESHA UOTO WA ASILI KUPITIA MRADI WA NATIVE PEP

Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) inatekelekeza mradi wa utafiti wa Mimea Asilia Kwa Watu na Mazingira (NATIVE PEP _Native Plants for Environment and People) ambao unatekelezwa nchini Tanzania katika mikoa ya Arusha (Wilaya ya Longido, Kijiji cha Tingatinga) na Kilimanjaro (Wilaya ya Siha, Kijiji cha Mawasiliano). Utafiti huu unalenga kutatua changamoto za kuenea kwa mimea vamizi, hali inayochochewa na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na ukataji wa miti hovyo pamoja na wingi wa mifugo.

Mradi huu unatekelezwa na TAFORI kwa kushirikiana na wadau kama Shirika la CABI Swiziland na Afrika, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) na Serikali za Mkoa, Wilaya na vijiji. Kupitia mradi huu, jamii za wakulima na wafugaji zimepewa mafunzo juu ya namna ya kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira unaotokana na kuenea kwa mimea vamizi na ukataji wa miti hovyo.

TAFORI ikishirikiana na wadau wake ilitoa mafunzo kwa vitendo kwa washiriki takribani ya 80 wakiwemo viongozi wa vijiji, kamati za mazingira, kamati za malisho, maafisa ugani wa kata na vijijini wa Kijiji hicho.  Aidha mradi huu imetoa elimu kwa wanakijiji kuhusu namna ya kuvuna majani, kutenga na kuyatunza kwa ajili ya mifugo.Taasisi imekua ikifanya tafiti ya kurudisha uoto wa asili ili kupunguza uvamizi wa kuenea kwa mimea vamizi katika ardhi ya Tanzania.

Akizungumza kama kiongozi wa mradi huu Mtaalamu wa Utafiti kutoka TAFORI Bw. Dikson Xavery alisema “mradi huu umeanzisha majaribio sita ya kurudisha uoto wa asili katika Kijiji cha Tingatinga na mawasiliano, na kuweza kutoka mbegu za kuzalisha  majani ya asili kwa wananchi takribani 40 wa vijiji hivyo”.

Wananchi wameipongeza na kushuru utekelezaji wa mradi wa utafiti huu kwa kutoa mafunzo hayo kwani wamewapa matumaini ya namna watakavyoweza kukabiliana na changamoto hizo na kuepukana na vifo vya mifugo.

“Tunashukuru kwa kutupatia mbegu na elimu hii na sisi tumeshatenga maeneo yetu kwaajili ya kurudisha uoto wa asili uliopotea” alisema Mariam Laizer mmoja wa wanakiji aliepata mafunzo hayo”.