SIFA ZA ASALI YA TANZANIA, ALAMA YA UTAMBULISHO NDANI NA NJE YA NCHI.

Matokeo ya utafiti yaliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania TAFORI katika kubaini sifa za asali kwenye uoto mbalimbali hapa nchini yamebaini uwepo wa asali yenye sifa tofauti katika ubora ikiwemo ladha, rangi pamoja na viambata muhimu. Uwepo wa sifa hizi za asali umewezesha kutengenezwa kwa Alama ya Asali ya Tanzania (Honey Trademark) itakayoitambulisha asali hii ndani na nje ya nchi.

Haya yameelezwa na Mhe. Balozi Dk. Pindi Chana Waziri wa Maliasili na Utalii wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika Mwaka wa Fedha 2024/25, katika Kikao cha 27 cha Mkutano wa 19 wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, amesema Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) imefanya tathmini yakubaini kiwango cha asali kinachozalishwa katika mizinga kupitia manzuki 21 ya majaribio ya kisayansi zilizofanywa katika Halmshauri za Wilaya za Kongwa, Chamwino, Manyoni, Sikonge, Kasulu, Mlele, Bukombe, Butiama, Itilima, Morogoro, Kibiti, Handeni, Pangani, Mtama (Rondo), Tunduru, Mufindi, Njombe, Chunya, Siha, Same na Simanjiro.

Amesema, matokeo ya awali ya utafiti huu yanaonesha wastani wa uzalishaji wa Kilogramu 19.10 za asali kwenye mzinga wa nyuki wa kisasa ukilinganishwa na Kilogramu 10 zinazozalishwa katika mizinga ya kienyeji, na hivyo,

Taasisi kupitia matokeo haya inachochea jamii kutumia mizinga ya kisasa ili kuongeza kiwango na ubora wa mazao ya nyuki.Kupitia utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2025/26, Waziri Chana amesema, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) imejipanga kufanya utafiti wa namna bora ya kutumia tasnia ya ufugaji nyuki kuboresha utalii wa nyuki (API-TOURISM) na kuanzisha manzuki za utafiti na mashamba ya kuzalisha mazao ya nyuki katika mikoa ya Dodoma, Shinyanga na Singida.

Kadhalika, Waziri Chana amewakaribisha Wabunge wote na wadau wa sekta ya Maliasili na Utalii kushiriki katika Maonesho ya Siku ya Nyuki Duniani ambayo yanaendelea kufanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma yanayotarajiwa kuhitimishwa Mei 20, 2025.