TAFORI, CHINA ZABAINI FURSA ZA USHIRIKIANO KATIKA UTAFITI WA MISITU NA UFUGAJI NYUKI

Dodoma. Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) na ujumbe wa Wataalamu wa misitu kutoka China wameanza majadiliano ya kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu katika tafiti, uhifadhi na kukuza utalii wa misitu, ikiwamo kuanzisha bustani ya mimea na kufanya utafiti wa spishi adimu na zilizohatarini kutoweka duniani

Ujumbe huo kutoka Jimbo la Hunan, ambao uko nchini kwa ziara maalumu, ulitembelea TAFORI jana Novemba 13, 2025, kwa lengo la kufahamu majukumu ya Taasisi na kutambua maeneo yenye fursa za ushirikiano wa kisayansi.

Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dk. Revocatus Mushumbusi, alisema Taasisi yake imejikita katika kufanya tafiti za misitu na ufugaji nyuki, kuhifadhi taarifa za rasilimali za kiasili na kubuni teknolojia za kuongeza tija katika usimamizi wa misitu, hivyo iko tayari kushirikiana na China katika maeneo ya utafiti, uvumbuzi na uhamishaji teknolojia.

 

Naye Mkurugenzi wa Utafiti wa Misitu TAFORI, Dk. Chelestino Balama, alieleza kwa undani kazi za taasisi hiyo, akitaja fursa kama kuanzisha bustani za mimea, tafiti za pamoja za mimea adimu na kubadilishana takwimu za kisayansi kati ya taasisi hizo mbili.

Kwa upande wa ujumbe wa China, Kiongozi wa msafara ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Jimbo la Hunan, Jianga Rui, alisema wamelenga kujifunza mifumo ya uhifadhi ya Tanzania na kutafuta miradi ya pamoja itakayojenga uhusiano wa kirafiki na kukuza utafiti, uhifadhi na utalii wa misitu.

Alisema baada ya kurejea China, watapeleka taarifa kwa mamlaka husika ili kuratibu maandalizi ya rasimu ya makubaliano yatakayowezesha kuanza kwa hatua za ushirikiano.