Siha, Kilimanjaro | Julai 16, 2026 Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), kwa kushirikiana na CABI na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), imeimarisha juhudi za urejeshaji wa uoto wa asili kwa kuanzisha ushirikiano na Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilimanjaro na Shule ya Msingi Mawasiliano wilayani Siha kupitia Mradi wa Utafiti wa Mimea ya Asili kwa Watu na Mazingira (Native PEP).
Ushirikiano huo unalenga kuwashirikisha walimu na wanafunzi katika shughuli za urejeshaji wa mazingira kwa kutumia mimea ya asili, huku ukijenga kizazi chenye maarifa, stadi na uwajibikaji katika usimamizi endelevu wa rasilimali za asili.
Akizungumza wakati wa kikao cha majadiliano kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kiongozi wa Mradi wa Native PEP kutoka TAFORI, Bw. Dickson Xavery, alisema shule ni jukwaa muhimu la kuandaa kizazi kitakachosimamia rasilimali za asili kwa maarifa na uwajibikaji.
“Tunapowawezesha wanafunzi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za urejeshaji wa mazingira, tunajenga msingi wa jamii yenye uwezo wa kulinda na kusimamia rasilimali za asili kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Bw. Xavery.
Katika kuimarisha ushirikiano huo, timu ya mradi ilisisitiza umuhimu wa kujifunza kwa vitendo ili kuwawezesha wanafunzi kujenga uelewa, umiliki na uwezo wa kuhamisha maarifa ya uhifadhi wa mazingira kwa familia na jamii.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Elimu ya Walimu Bern nchini Uswisi, Prof. Michele Notari, alisema wanafunzi hujifunza kwa ufanisi zaidi wanaposhiriki moja kwa moja katika shughuli za vitendo kuliko kutegemea nadharia pekee.
Alisema maarifa watakayopata shuleni yatawafikia pia wazazi na jamii kupitia wanafunzi hao, hatua itakayochochea umiliki wa shughuli za uhifadhi wa mazingira katika ngazi ya jamii.
Majadiliano hayo yalizaa makubaliano ya kuanzisha Vilabu vya Native PEP, vitalu vya miche ya miti ya asili, uzalishaji wa nyasi za malisho, upandaji wa miti ya matunda pamoja na utekelezaji wa shughuli za eneo la hifadhi lisilo na uzio (Social Fence) zitakazohamasisha jamii kushiriki katika kulinda maeneo yanayorejeshwa.
Aidha, kupitia ushirikiano huo, mradi utafadhili ujenzi wa mfumo wa kuhifadhi maji katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilimanjaro ili kusaidia shughuli za utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wao, Walimu waliupokea mradi huo kwa furaha na kuahidi kutoa ushirikiano huku wakipendekeza kuanzishwa kwa vitalu vya mimea tiba ya asili, ufugaji wa nyuki wasiodunga na kuhakikisha kila mwanafunzi anamiliki na kutunza mti wake binafsi.