TAFORI YATOA ELIMU YA UTAFITI KUONGEZA TIJA KATIKA MASHAMBA YA MITI NANENANE

Nanenane, Morogoro. Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) imeendelea kutumia Maonesho ya Wakulima Nanenane, kuwaelimisha wakulima wa mashamba ya miti kuhusu matumizi ya matokeo ya utafiti katika kuongeza ubora na tija ya shughuli zao.

Kupitia maonesho hayo, TAFORI imetoa elimu kwa wadau kuhusu umuhimu wa kuzingatia umri sahihi wa uvunaji wa miti, ili kupata mbao zenye ubora zinazoweza kutumika katika ujenzi na utengenezaji wa samani.

Aidha, wadau wamepatiwa elimu kuhusu namna ya kutambua na kukabiliana na magonjwa yanayoweza kusababisha miti kudhoofika, kukauka, pamoja na kanuni za msingi za upandaji na utunzaji wa miti kwa kuzingatia aina ya udongo na mazingira ya eneo husika.

TAFORI imeeleza kuwa matokeo ya tafiti yanaonesha umuhimu wa kuzingatia eneo linalofaa kwa kila aina ya mti, kwa kuwa si kila aina ya mti inafaa kupandwa katika kila eneo. Uelewa huo unalenga kuwasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi wa aina za miti na maeneo ya kuipanda.

Maonesho ya Nanenane yanaongozwa na kaulimbiu “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050”