
Urusi imejipanga kufanya mashirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) katika tafiti za kisayansi, elimu kwenye sekta ya Misitu Tanzania.
Haya yamezungumzwa Machi 11, 2025, katika kikao kilichofanyika TAFORI Makao Makuu, Morogoro baina ya Wanasayansi na Wataalamu wa utafiti kutoka nchini Urusi na TAFORI, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kubaini maeneo ya utaifiti wanayoweza kushirikiana kupitia sekta ya Misitu.
Kadhalika, mashirikiano haya yamelenga kubaini na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabali sekta ya Misitu nchini ikiwamo kupata uzoefu wa mbinu za kukabiliana na majanga ya moto, uzajilishaji wa mazao na ufuatiliaji wa maendeleo ya Misitu pamoja na kubaini magonjwa katika mimea kupitia teknolojia za kisasa kamavile satellite na ndege nyuki(drone).
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amesema kuwa mashirikiano haya yatawezesha Watalaamu wa utafiti kutoka TAFORI na vyuo vikuu vya elimu ya Misitu nchini kufaidika kielimu, kupata uzoefu katika matumizi ya sayansi na teknolojia katika sekta ya misitu.
“Wenzetu katika eneo la sayansi ya Misitu wamekwenda mbali katika matumizi ya sayansi na tekinolojia, kwa kupitia uzoefu walio nao tunaona kwamba tutafaidika kwa kiasi kikubwa,”
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) Dkt. Revocatus Mushumbusi amesema kupitia mashirikiano haya Wataalamu wa utafiti katika Taasisi wataweza kubadilishana uzoefu na Wataalamu kutoka nchini Urusi katika kupata uzoefu na kujifunza namna ya kutumia tekinolojia za kisasa katika kukabiliana na majanga ya moto Msituni, ikiwa ni pamoja na kuwa na tafiti za pamoja zitakazoleta suluhisho katika sekta ya Misitu nchini.
“Tumejifunza teknolojia wanazozitumia katika kubaini na kuweza kuzuia majanga mbalimbali ya misituni, na sisi tutaendelea kujifunza na mwisho tutakuwa na tafiti za pamoja ambazo zitatusaidia kukabiliana na changamoto katika sekta ya Misitu nchini,”
Mashirikiano haya yanavileta pamoja vyuo vikuu vya Misitu Tanzania na Taasisi za Utafiti na vyuo vikubwa nchini Urusi kwenye maeneo ya utafiti katika namna ya kufaidika na hewa ukaa, afya ya udongo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Lakini pia kubadilishana kwa Wataalamu kutoka nchini kwenda Urusi kupata elimu na maarifa katika sekta ya misitu, kupata masamo ya muda mrefu na fursa kwa nchi zote mbili katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za Misitu.