
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paul Matiko Chacha amewataka Wananchi wanaotoka ndani na nje ya Mkoa wa Tabora kutumia fursa ya Warsha ya Kitaifa ya Uyoga Mwitu unaoliwa na Binadamu iliyo andaliwa na Shirika la ADAP, Adansonia Consulting kwa kushirikiana na TAFORI kupata uzoefu na uwezeshwaji katika kukuza mnyororo wa thamani wa uyoga mwitu unaoliwa kama chakula, dawa za jadi na chanzo cha mapato.
Akifungua Warsha hiyo Mkoani Tabora, Februari 27, 2025 katika ukumbi wa Isiki Mwanakiyungi Hall, Mkuu wa Mkoa wa Tabora akiwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Cornel Magembe, amesema kutokana na changamoto zinazoikabili sekta hii ya kukuza uyoga mwitu unaoliwa amewaasa washiriki kutumia fursa ya jukwa hilo kupata utaalamu, uzoefu na ubunifu katika kufungua njia na kukuza sekta ya uyoga nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora amewataka waandaji wa mradi huu kuwaandaa washiriki wa Warsha ya Uyoga Mwitu Unaoliwa na Binadamu, kwa kuwawezesha katika uvunaji, kuwajengea uwezo na kuwawezesha katika upatikanaji wa masoko na kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta hii.
Ametoa rai kwa TAFORI kuendelea na Utafiti na utambuzi na uzalishaji wa uyoga mwitu wa aina mbalimbali kwaajili ya kuongeza upatikanaji wake kwa uhakika wa chakula nchini na kushirikisha matokeo katika warsha za umma.
Mradi huu ulioanzishwa na ADAP, Adansonia Consulting kwa kushirikiana na TAFORI unaoendana na dira ya Taifa ya mwaka 2025 Tanzania version 2025 na Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini The National Strategy for Growth and Deduction of Poverty unatarajiwa kufungua fursa za kiuchumi na kukuza mnyororo wa thamani wa sekta ya uyoga mwitu unaoliwa nchini.