WENYEKITI NA WATENDAJI WA VIJIJI 22 WATAKIWA KUSIMAMIA UHIFADHI WA MAZINGIRA NA VYANZO VYA MAJI

KIBONDO| Septemba 17, 2026: Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Kanali (Mstaafu) Mhe. Aggrey Magwaza, amewataka wenyeviti na watendaji wa vijiji 22 katika Wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko kusimamia uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kanali (Mstaafu) Magwaza ametoa wito huo leo Wilayani Kibondo wakati akifungua awamu ya pili ya mafunzo kwa wenyeviti na watendaji wa vijiji 22 kutoka wilaya hizo, yanayohusu “Ujumuishaji wa Ustahimilivu Unaotegemea Mifumo Ikolojia (EbA) na Urejeshaji wa Mandhari katika Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi ya Vijiji Inayohimili Mabadiliko ya Tabianchi.”
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), kwa ufadhili wa Green Climate Fund (GCF).
Amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa GCF FP218, “Kujenga Uhimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi katika Mandhari za Mkoa wa Kigoma, Tanzania”(Building Climate Resilience in the Landscapes of Kigoma Region, Tanzania).
Kanali (Mstaafu) Magwaza, amesema mradi huo unalenga kuimarisha uwezo wa jamii na taasisi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia usimamizi endelevu wa ardhi, misitu na mifumo ikolojia.
Aidha, amekemea uchomaji moto holela katika vijiji vya Wilaya za Kasulu, Kibondo na Kakonko, akisema vitendo hivyo vinaharibu mifumo ikolojia.
Amewataka viongozi hao kuachana na imani potofu kuhusu uchomaji moto katika maeneo ya misitu ya asili na kusimamia udhibiti wa mioto hiyo, ikiwemo katika mashamba ya miti.
Kanali (Mstaafu) Magwaza pia amewaasa washiriki kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kujifunza kwa vitendo na kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu yao ya usimamizi wa mazingira na matumizi ya ardhi.